Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, ameshiriki katika warsha maalumu ya elimu iliyofanyika leo katika ukumbi wa Al-Mustafa University International, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, ambapo aliwasilisha mada iliyokuwa na anuani isemayo “Asili ya Maendeleo na Tamaduni za Kimagharibi na Jinsi ya Kuzifahamu.”
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wanafunzi, wahadhiri pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za kielimu na kidini, ikilenga kujadili namna jamii za Kiislamu zinavyoweza kujitambua kiutamaduni katika ulimwengu unaokabiliwa na wimbi la mabadiliko ya fikra na mfumo wa maisha wa Kimagharibi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Maulana Sheikh Jalala alielezea kuhusu maendeleo ya kweli kwamba; hayawezi kupimwa kwa mizani ya mali na teknolojia pekee, bali hupaswa kujikita katika msingi wa maadili, utu na uhusiano sahihi kati ya binadamu na Muumba wake. Alibainisha kuwa historia ya maendeleo ya Kimagharibi imejengwa katika msingi wa fikra za kibepari na usekula ambazo mara nyingi huzingatia manufaa ya mtu binafsi zaidi ya maslahi ya kijamii.
“Ni muhimu kwa vijana wetu kufahamu kuwa maendeleo ya kimagharibi, pamoja na mchango wake katika teknolojia na taaluma, yamekuwa pia chanzo cha kuenea kwa fikra zinazopunguza nafasi ya dini katika maisha ya kila siku. Hivyo ni jukumu letu kama Waislamu kuyachambua kwa uangalifu na kujifunza yaliyo mazuri bila kupoteza utambulisho wetu wa Kiislamu,” miongoni mwa mambo yaliyo ashiriwa kwenye warsha hiyo.
Vile vile palisisitizwa kuwa: Elimu ndio chombo kikuu kinachoijenga jamii yenye mwamko wa kielimu na kiroho, taasisi za Kiislamu zinapaswa kuwekeza zaidi katika tafiti na mitaala inayochochea fikra za kimaendeleo zenye misingi ya Kiislamu.
Vilevile, wanafunzi wa vyuo vya Kiislamu nchini Tanzania, walihimizwa kujikita katika kujenga uelewa mpana wa falsafa za kimataifa ili waweze kuzitathmini kwa misingi ya Qur’ani na Sunna.
Hafla hiyo pia ilipambwa na uwepo wa wageni kutoka taasisi rafiki za elimu ya Kiislamu pamoja na wawakilishi wa vyuo mbalimbali vya dini vilivyopo Dar es Salaam.
Kwa ujumla, warsha hiyo imeonekana kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana fikra na kuchochea mjadala mpana kuhusu namna Waislamu wa Tanzania na Afrika Mashariki wanavyoweza kushiriki katika maendeleo ya dunia bila kupoteza misingi ya utamaduni na imani zao.
Maoni yako